VRB Yawanoa Wathamini Kupitia Mafunzo ya Uchambuzi wa Taarifa za Kifedha

Imewekwa: 15 July, 2025
VRB Yawanoa Wathamini Kupitia Mafunzo ya Uchambuzi wa Taarifa za Kifedha

Bodi ya Usajili wa Wathamini (Valuers Registration Board - VRB) imefanikiwa kuandaa mafunzo ya siku mbili kwa wathamini, yaliyolenga kuongeza uelewa na umahiri katika uchambuzi wa taarifa za kifedha kwa ajili ya uthamini wa kampuni au biashara.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo FRV. Zidikheri Mndeme amefungua mafunzo hayo tarehe 12 Juni 2025 katika Ukumbi wa PSSSF, Millenium Towers, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, FRV.  Mndeme alieleza kuwa uelewa wa taarifa za kifedha ni msingi muhimu kwa wathamini katika kufanya tathmini yenye ufanisi, hasa katika mazingira ya sasa ya kiuchumi yanayobadilika kwa kasi.

‘‘Washiriki watajifunza mbinu za kisasa za kusoma, kuchambua na kutumia taarifa za kifedha katika kufanya tathmini sahihi za kibiashara’’ alisema Mndeme.

Kwa upande wao, washiriki walionyesha kuridhishwa na mafunzo hayo ambapo walikiri kuwa yatawasaidia katika kuongeza ufanisi utakao endana na mahitaji ya soko pamoja na kuboresha uaminifu katika taaluma hiyo.

Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za Bodi ya Usajili wa Wathamini kuhakikisha wathamini wanakuwa na ujuzi wa kisasa unaowawezesha kutoa huduma bora na zinazozingatia viwango vya Kimataifa.

Settings