emblem

The United Republic of Tanzania

VALUERS REGISTRATION BOARD

BODI YA USAJILI WA WATHAMINI TANZANIA (VRB) YAENDESHA MAFUNZO YA USAJILI WA KUDUMU KWA WATHAMINI 121


Bodi ya Usajili wa Wathamini Tanzania (VRB) imeendesha mafunzo ya usajili wa kudumu wa wathamini 121 ambao wataenda kunufaika na usajili wa kudumu na kuweza kupata fursa ya kujitegemea katika kujiajiri.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo Mthamini kutoka Bodi ya Usajili wa Wathamini Tanzania (VRB), FRV Christopher Kilatu amesema Mafunzo hiyo ni ya wiki tatu darasani ambapo wanafunzi watajifunza kozi mbalimbali ambazo zitaweza kuwafanya waweze kufaulu na kuweza kupata usajili wa kudumu.

"Wakishajifunza darasani kutakuwa na zoezi la wanafunzi kwenda kufanya uthamini kwa vitendo na baadae watafanya mawasilisho (presentation) ya hizo kazi zao na watakaofaulu watakuwa wamehitimu mafunzo yao ya usajili wa kudumu na kupewa vyeti". Amesema FRV Kilatu

Amesema Mafunzo hayo ni ya wathamini ambao tayari wameshasajiliwa na bodi na wanataka kuhama kutoka usajili wa awali kwenda kwenye usajili wa kudumu.

Aidha amesema Mafunzo hayo yanakwenda kupanua wigo kwa wathamini katika kufanya kazi zao, kwasababu kisheria wathamini wakiwa katika usajili wa ngazi za awali hawawezi kufanya kazi wao wenyewe mpaka wasimamiwe.

"Hawa wanaosoma haya mafunzo sasa hivi wakishahitimu na kufaulu watapata usajili wa kudumu hivyo wanaweza kwenda kufanya kazi wao wenyewe na kuwapa fursa ya kuweza kufungua kampuni na kusimamia kazi mbalimbali, amesema Kitalu"

Kwa upande wake Glory Tesha ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo amesema watanufaika kwa ujuzi ambao watapatiwa na vilevile wataweza kujiajiri kwani wathamini mara nyingi sokoni wanakuwa na ushindani hasa makampuni ambayo mwanzoni yalikuwa ni machache lakini kwa sasa mafunzo hayo ni njia nzuri kwa wathamini wadogo kuweza kujiajiri.

Nae Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo PRV Petro Michael amesema kupitia mafunzo hayo watapata ujuzi ambao utawasaidia kulitumikia taifa kwa ujumla kwani idadi ya wathamini wanaoshiriki katika mafunzo hayo ni kubwa na matumaini yao ni kuona wote wanafaulu na kupatiwa vyeti.